Na Alison Gorman, M.D.

Je, umesikia kuhusu Kifua Kikuu? Kifua Kikuu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria ya kifua kikuu. Ugonjwa huu unapatikana sana sehemu nyingi za dunia. Watu wenye kifua kikuu wanaweza kuwa na maambukizi wazi, ambayo yanaweza kuwafanya wajisikie wagonjwa sana, au wanaweza kuwa na maambukizi ya kimya, yanayoitwa Latent TB au “Kifua Kikuu kilicholala,” ambayo haina dalili yoyote.
Maambukizi ya bakteria ya Kifua Kikuu ni kupitia kupumua kijidudu kutoka kwa hewa. Hii mara nyingi hutokea wakati mtu anapumua hewani baada ya mtu mwenye Kifua Kikuu kueneza bakteria kwa kuzungumza, kuimba, au kukohoa.

Dalili za Kifua Kikuu wazi ni kikohozi kisichoisha, kutokwa na jasho usiku, homa, au kupungua uzito. Kwa kawaida, watu walio na maambukizi ya Kifua Kikuu hawajisikii vizuri.
Kinyume na dalili hizo, mtu aliye na maambukizo ya Kifua Kikuu Kimya(Latent TB) anahisi afya kwa sababu bakteria wamelala na hawasababishi dalili zozote. Mtu aliye na Kifua Kikuu cha Kimya hawezi kueneza viini vya Kifua Kikuu kwa wengine.
Ni kitu cha muhimu kujua kama mtu ameathiriwa na viini vya Kifua Kikuu. Tunafanya hivyo kwa mtihani wa ngozi unaoitwa “PPD” au mtihani wa damu. Zote mbili zinaonyesha ikiwa mtu amepumua vijidudu vya Kifua Kikuu.
Kufuatana na matukio ya kipimo, ikiwa mtu amepumua kiini cha TB, ni muhimu kujua ikiwa kidudu kimelala au kiko hai. Kwa sababu Kifua Kikuu kwa kawaida husababisha dalili kwenye mapafu, wahudumu wa afya hukagua Eksirei ya mapafu ili kuhakikisha kuwa bakteria haijasababisha ugonjwa wowote. Pia watauliza kuhusu dalili nyingine kwa sababu Kifua Kikuu kinaweza kuathiri sehemu nyingine za mwili pamoja na mapafu.
X-ray inapoonyesha ugonjwa hai, wagonjwa hutumwa kwa mtaalamu wa Kifua Kikuu kupata matibabu na dawa kali. Ni muhimu kwa wagonjwa hawa kutibiwa – inalinda afya zao, na pia kuwazuia kueneza virusi kwa watu wengine katika jamii. Wagonjwa walio na Kifua Kikuu hai hufanya kazi na timu ya matibabu ili kuhakikisha wanapata dawa na utunzaji wanaohitaji. Kawaida matibabu hudumu kwa miezi kadhaa.
Kinyume na hiyo, ikiwa X-ray haionyeshi ugonjwa wowote katika mapafu na hakuna wasiwasi kwa Kifua Kikuu mahali pengine katika mwili, mtu ana maambukizi ya Kifua Kikuu cha Kimya. Ni muhimu kwa watu walio na maambukizi ya Kifua Kikuu cha Kimya kupata matibabu, pia. Huenda wengine wakashangaa kwa nini mtu anahitaji kutibiwa ikiwa anahisi vizuri; hii ni kwa sababu bakteria wanaolala wanaweza kuamka wakati wowote na kusababisha maambukizi hai. Hii hutokea kwa 5-10% ya watu. Bakteria hao wakiamka, watu wanaweza kuhisi wagonjwa na kisha wanaweza kusambaza virusi kwa wengine. Wagonjwa walio na Kifua Kikuu cha Kimya huchukua dawa kwa miezi kadhaa ili kuhakikisha kuwa bakteria hawaamki kamwe.
Kupima pamoja na matibabu ya Kifua Kikuu hai ama cha Kimya hutunufaisha sote. Tunaposhirikiana kuzuia kuenea kwa kifua kikuu, afya ya watu binafsi na jamii yetu inaboreka. Tafadhali zungumza na timu yako ya matibabu ikiwa una maswali au unataka kuchunguzwa kwa kifua kikuu.