Na Patrick Nduwimana

Maine ni moja ya majimbo ya Marekani yenye masharti magumu ili kupata leseni ya kufungua saluni ya kinyozi. Ili upewe leseni na Mamlaka husika, unatakiwa kulipa ada ya kati ya dola elfu 13 na miya sita na dola elfu kumi na nne na miya tano($13,600-$14,500) na kukamilisha mafunzo ya saa 800 ya kunyoa nywele kwenye shule ya masomo ya ufundi na saana ya urembo. Iwapo huna uwezo wa kulipa ada hiyo, njia nyingine ni kufanya kazi ya kunyoa katika saluni inayomilikiwa na mtu aliyepewa kibali na mamlaka ya jimbo la Maine kwa kipindi cha mwaka mmoja, sawa na masaa 1,600 ya kazi.

Baada ya hapo, mmliki wa saluni anathibitisha kwa maandiko kwamba umekamilisha masaa hayo 1,600, kisha unafanya mtihani wa jimbo wa kupata leseni. Yves Karubu, muhamiaji raia wa Burundi anaeishi katika mji wa Portland jimbo la Maine alitumia njiya hiyo ya pili.

Alianza Kufanya Kazi ya Kinyozi Nchini Burundi Akiwa Bado Mdogo

Yves alikuwa na kipaji cha kuchora tangu akiwa mdogo. Ni mzaliwa wa mtaa wa Cibitoke, kaskazini mwa jiji la Bujumbura, anasema alikuwa anapenda kuchora nyuso na vicwa vya wanaume wanaotoka saluni kunyolewa ndevu na nywele. Hilo ndilo lilimchochea kwenda kuomba kazi ya kinyozi katika saluni moja mtaani Cibitoke, akiwa na mri wa miaka 12 na akiwa mwanafunzi wa shule  ya upili.

Kimo chake na umri wake mdogo ilikuwa changamoto kwa sababu mmiliki wa saluni hiyo hakuamini jinsi mtoto mfupi mdogo anaweza kumuomba kazi ya kinyozi.

Yves hakuvunjika moyo, alitafuta mbinu ili mmiliki wa saluni amuamini na aone kwamba kijana huyo mdogo anayo nia ya kufanya kazi.

“Mwenye saluni akimaliza kunyoa nilikuwa nafyagia, naondoa taka za nywele. Akija asubuhi kuanza kazi, alikuwa anakuta nimesafisha mashine za kunyoa na vioo. Siku moja, kutokana na shughuli nyingi alizokuwa nazo, boss wangu aliniomba ninyowe mteja ili ahakiki kwamba najua kufanya kazi. Alishangaa kuona jinsi nilvyomnyoa vizuri mteja huyo, na hapo ndipo alianza kuniamini na kuniajiri,” Yves ameiambia Amjambo Africa.

Licha ya umri wake mdogo, wateja walianza kumuamini. Akitoka shule, saa tisa alasiri baada ya kupumzika, alikuwa anajielekeza kwenye saluni hiyo na kukuta mlolongo wa wateja wanaomsubiri ili awanyowe.

Picha | Yves Karubu

Mwenye saluni aliridhika na kumuajiri rasmi. Yves alikuwa anaanza kazi saa tisa alasiri hadi saa tatu usiku, akifika nyumbani anapitia masomo ya darasani na asubuhi anajielekeza shuleni, saa tisa alasiri anaelekea saluni kunyoa, hiyo ndiyo ilikuwa ratiba yake.

Wamiliki wengine wa saluni katika mtaa wa Cibitoke walipata taarifa za kinyozi mdogo mchapakazi na mwanafunzi na kumuomba afanye nao kazi kwa ahadi ya kumuongezea mshahara. Yves anasema boss wake wa kwanza alikuwa anamlipa mshahara wa asilimia 30 ya kipato cha kila siku. Baadaye alipata boss mwingine aliyekubali kumlipa asilimia 40 ya kipato, hivo ndivyo alivyoamua kuhamia kwenye saluni hiyo nyingine baada ya kufanya kazi na boss wake wa zamani kwa  miezi mitano.

Boss wake wa pili alifurahishwa sana na utendaji kazi wa Yves na kumteua kuwa kiongozi wa wafanyakazi wengine.

“Nilikuwa nanyoa wateja wengi kuliko wafanyakazi wenzangu, baada ya kuona kwamba ninachangia sana kwa kuongeza mapato, boss wangu alinipandisha cheo.”

ADVERTISEMENT

Yves aliendelea kuwa kivutio cha saluni nyingine. Mmliki mwingine wa saluni aliahidi kumpa asilimia 45 ya mapato ya kila siku, na baadaye akahamia kwenye saluni hiyo ya tatu. Hapa alifanya kazi kwa miaka miwili.

Yves alikuwa na ndoto ya kumiliki saluni yake. Alishauriana na mfanyakazi mwenzake katika saluni hiyo ya tatu ili watafute mtaji wa kuanzisha saluni yao. Mwenzake alimwambia yuko na laki sita (600,000) pesa ya Burundi. Pesa hiyo ilikuwa inatosha kukodi nyumba ya vyumba viwili: Chumba kimoja kama saluni ya kinyozi,  chumba kingine kama malazi.

Yves alileta mtaji wa laki nne (400.000).

“Niliuza baiskeli yangu laki 1 na elfu tisini (190,000), laki mbili na elfu 10 (210,000) zilizokuwa zinabaki nilipewa na rafiki yangu mzungu. Hivo tukapata mtaji wa miliyoni moja (1,000,000) na kufungua saluni yetu.”

Anasema walianza na saluni ndogo, baada ya miaka miwili walifungua saluni kubwa kidogo, na kuipa jina la Mimosa Salon. 

“ Mimosa ilikuwa saluni yenye umaarufu sana katika mtaa wa Cibitoke. Kwenye bango, kulikuwa kumeandikwa Mimosa Salon Yves and Stany. Tulianza na mashine tatu, viti viwili, vioo viwili na mfyagio mmoja.”

Yves na mwenzake walifanya kazi pamoja katika saluni yao kwa miaka minne. Mshiriki wake alimuomba wauze saluni hiyo, kwa sababu alikuwa na mpango wa kwenda Afrika Kusini kuanza maisha mapya. 

“ Kipindi hicho nilikuwa nahitimu masomo yangu ya sekondari, ili nisiwe pingazi kwa mipango yake tuliuza saluni.”

Yves anasema baada ya kuuza saluni hiyo, alinunua mashine mpya, baiskeli mpya na vifaa vingine vya kumuwezesha kufanya kazi yake ya kinyozi. Wakati huo alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha kibinafsi, Universite des Grands Lacs katika kitengo cha masomo ya saikolojia ya kijamii na matibabu.

Alisaini mikataba na wafanyakazi wa baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs), maafisa wa serikali, mawaziri na wabunge.

“Nilikuwa nawakuta majumbani kwao kila  Ijumaa na Jumamosi na kuwanyoa. Nilikuwa nanyoa watu 40 ndani ya siku mbili. Hivo ndivyo niliendelea kupata mapato katika kazi yangu ya kinyozi wa kujitegemea.”

Safari Yake ya Kuja Marekani na Kuwa Kinyozi

Yves pia ni mpiga ngoma. Yeye na kundi la wapiga ngoma wenzake walikuwa wanapata mwaliko wa kwenda kutumbwiza  ngoma katika nchi za kigeni. Walisafiri sana kwenda kupiga ngoma katika nchi kama Kenya, nchi za Ulaya na Asia. Mwaka wa 2013, walialikwa kwenye mashindano ya tamasha la kitamaduni Korea Kusini na tunukiwa tuzo iitwayo Grand Prix.

Mwaka 2015 walipata mwaliko wa kuja kupiga ngoma Marekani, katika jimbo la Ohio kushiriki tamasha la kitamaduni wakapewa pia tuzo. Wakiwa bado Marekani, Burundi ikakumbwa na mzozo wa kisiasa. Yves na wenzake walisubiri kwa matumaini kwamba hali nchini mwao inaweza kuwa shwari ili warudi nyumbani. Lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo waliamua kubaki Marekani, katika jimbo la Maine.

Baada ya muda mchache akiishi Maine, Yves aligundua kwamba jimbo  hili lina wahamiaji wengi kutoka Burundi, Rwanda, Congo  na hapo akaona kuwa akianza kazi ya kinyozi atapata wateja wengi. Alianza mchakato wa kuomba hifadhi, baada ya miaka michache alipewa hifadhi na mwaka 2022 alipata uraia wa Marekani.

“Nilipopata hifadhi, niliuliza kinachohitajika ili nianze kazi ya kinyozi. Niliambiwa kwamba kabla ya kuwa kinyozi lazima uende shule na usome kwa miezi mitano hadi miezi kumi na tatu na inakugharimu Karubu dola elfu 20. Sikuwa na uwezo huo.”

Kutokana na pingamizi hiyo, Yves alianza kunyoa watu katika nyumba anakoishi mjini Portland.

“Nilikuwa nanyoa watoto na watu wazima, na wateja walikuwa wengi.”

Leo Yves anafanya kazi katika majumba yanayohudumia watu wenye matatizo ya afya ya akili na anafanya pia kazi siku tatu kwa wiki kama mwanafunzi mwenye leseni ya kinyozi katika saluni katika mji wa Biddeford. Ni katika mchakato wa kukamilisha masharti ya jimbo la Maine kwa kufanya kazi masaa 1,600 katika saluni inayomilikiwa na kinyozi mwenye leseni na ambaye amekwisha fanya kazi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

“Ndani ya miezi mitatu ijayo, nitakuwa nimekamilisha masaa 1,600, kisha baadae nitafanya mtihani wa kupata leseni ya kinyozi.”

Yves anasema tayari amekwisha wasiliana na marafiki zake wenye taluma ya kunyoa ili baada tu ya kupata leseni, aanze mchakato wa kufungua saluni kubwa.

“Naelekea kukamilisha ndoto yangu ya kufungua saluni hapa Maine. Tayari nimekwisha jadiliana na marafiki zangu ambao wanajua kunyoa nikiwahimiza kutimiza masharti ya jimbo. Lengo ni kujiunga pamoja ili kufungua saluni kubwa ya kisasa.”

Yves anasema kazi kubwa itakayofuata akiwa na leseni mkononi, ni kutafuta mtaji au mkopo kwenye benki.

Wahamiaji kutoka nchi za kanda ya maziwa makuu na Afrika mashariki wanaomiliki saluni za kunyoa katika jimbo la Maine bado ni wachache.

Wahamiaji raia Burundi wanaoishi Maine wanakadiriwa kuwa sawa na zaidi ya 1,000 kulingana na shirika la jamii ya Warundi BCAM. Licha ya kuwa hakuna takwimu rasmi kuhusu idadi kamili ya wahamiaji kutoka Congo, raia wa  Congo ni miongoni mwa jamii kubwa ya wahamiaji kutoka Afrika waishio Maine.

“ Maine ina raia wengi sana kutoka Burundi na Congo. Tayari wateja wako, ninaamini kwamba nitakapofungua rasmi saluni nikiungana na wenzangu, biashara yetu itakuwa kwa kasi na tutapata mapato mengi.”