Na Jean Damascene Hakuzimana

Dozi elfu nane za chanjo za Johnson and Johnson ziliwasili Afrika Kusini mnamo Jumanne, Februari 16 na siku moja baadaye Afrika Kusini ilianza kuwapa wahudumu wa afya chanjo jijini Cape Town. Hii iliiletea matumaini nchi ya Afrika iliyoathirika zaidi na COVID – 19. Rais wa Afrika Kusini alishabikia kufika kwa chanjo kama hatua kubwa katika vita dhidi ya mrupuko wa COVID. Kwa juhudi za kutupilia mbali minong’ono ya uongo kuhusu chanjo hiyo, Rais Ramaphosa, waziri wa afya Mkhize na naibu waziri wa afya Phaahla walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuipokea chanjo hiyo. “Ichukue hii, ndipo sasa sote tuwe salama, na sote tuwe na afya nzuri,” Rais Ramaphosa aliwahimiza wananchi wenza. Afrika Kusini ndiyo nchi ya kwanza kupana chanjo ya Johnson and Johnson. Taifa hili lenye uchumi mkubwa limeathirika pakubwa na COVID 19, likiwa na zaidi ya vifo 48,000 pamoja na kusambaa kwa virusi hadi sasa inafanya taifa kuwa katika hali isiyo salama. Hata hivyo, Aljazera inaripoti kuwa chanjo kutoka Johnson and Johnson iliyo na uwezo wa takriban 57% na Novavax iliyo na uwezo wa takriban 50% zimedhihirishaa uwezo dhidi ya virusi ukilinganisha na chanjo nyingine. Afrika Kusini ina chanjo za Johnson and Johnson dozi milioni tisa baada ya kusimamisha makubaliano na chanjo za Oxford/AstraZeneca ambayo iligunduliwa kuwa na makali madogo kwa kulinganisha na chanjo mpya. Nchi inanuia kuchanja takriban watu milioni arobaini ambayo ni takriban 67% ya watu wote kufikia mwisho wa mwaka na ina dozi milioni 20 ya chanjo za Pfizer- BioNtech kuisaidia kutekeleza jukumu hilo. Mataifa mengine machache katika bara la Afrika yana mipango mizuri kama hiyo. Hata hivyo wanastahili kungojea COVAX – ambayo ni muungano wa kimataifa uliyoundwa kuhakikisha mgao ulio sawa wa chanjo kwa mataifa maskini – kutangaza mipango ya kuisambaza chanjo. Rwanda ilianza program ya chanjo mnamo Februari 14, kulingana na Reuters. Siku baada ya Rais Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe alitangaza kwenye twitter kuwasili kwa dozi 200,000 ziliyotengenezwa na kampuni ya Chinese National Pharmaceutical Company (Sinopharm). Zimbabwe inasema kuwa imetenga milioni $ 100 za kununua chanjo. Algeria, Morocco, Mauritius na Misri pia zimeanza kuwapa wananchi wao chanjo. Huku mataifa yaliyo na uwezo mkubwa yakiweka mikataba na kampuni za chanjo, Shrika la Afya Duniani [WHO] inaonya kuwa mikataba hii itaifanya chanjo za COVID- 19 kuwa ghali na muhali kupatikana kwa mataifa masikini ya Afrika. Ripoti za kipekee za Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa eneo la Afrika katika Shirika la Afya Duniani [WHO], alionya kwa kusema kuwa janga la Covid litakomeshwa na “ Sisi Kwanza badala ya Mimi Kwanza” . Programu ya COVAX ina mipango ya kutuma dozi bilioni 1.3 za COVID-19 kwa mataifa 92 yenye uchumi ndogo kufikia mwisho wa mwaka wa 2021. Mataifa mengine yameonyesha kutokuwa na haja ya kuweka mikakati ili kupata chanjo. Rais wa Tanzania, John Magufuli amekataa chanjo za COVID- 19. Kwa upande mwingine, Sauti ya Amerika inaripoti kuwa Seif Sharif Hamad, naibu rais wa kisiwa cha Zanzibar ya Tanzania aliaga Februari 17 baada ya wiki kadhaa za kuugua COVID- 19.